VICHWA MBALIMBALI

NGUVU YA DAMU YA YESU

Damu ya Yesu ina nguvu sana! Lakini je unajua ni kwa nini ilimwagika katika maeneo tofauti tofauti ya mwili wake?
Kwa mfano, tunasoma ya kuwa; “Hata zilipotimia siku nane za kumtahiri, aliitwa jina lake Yesu; …” (Luka 2:21). Tena imeandikwa katika wakolosai 2:11 ya kuwa: “Katika yeye mmetahiriwa kwa tohara isiyofanyika kwa mikono, kwa kuuvua mwili wa nyama, kwa tohara ya Kristo”.
Hii inaonyesha ya kuwa kutahiriwa kwa Kristo kulikuwa sii tu kwa ajili yake; bali ilikuwa pia kwa ajili yetu sisi tunaomwamini kama mwokozi wetu!
Na alipotahiriwa, damu yake ilimwagika! Jambo hili la kutahiriwa, lilianza wakati wa Ibrahimu (Kama ishara ya mtu kukubali kuingia katika agano na Mungu wa Ibrahimu)
Wakati wa kipindi cha Musa, jambo hili liliingizwa kama agizo la Torati. Hili ndilo lililowafanya “baadhi ya madhehebu ya Mafarisayo” waliokuwa wameokoka, kuwaelekeza wale wasiotahiriwa ya kuwa; “msipotahiriwa kama desturi ya Musa hamwezi kuokoka” (Matendo ya Mitume 15: 1,5)
Jambo la kutahiriwa au kutokutahiriwa kwa jinsi ya mwili, lilikuwa chanzo kikubwa sana cha malumbano na kutokushirikiana kwa Kanisa la Mwanzo
Mitume walijitahidi kulisuluhisha jambo hili waliloliita “Kongwa juu ya Shingo” (Matendo ya Mitume 15:10), kwa kuweka msisitizo wa damu ya Yesu kusafisha mioyo yetu, na kutupa tohara ya rohoni, na kutupa kukubalika mbele za Mungu kwa kufanana. Soma haya katika: Warumi 2: 25 – 29;, Waefeso 2: 11 – 13.
Damu ya Yesu inatupa kuingia katika agano jipya (Luka 22:20), na kutufanya uzao wa Ibrahimu kwa njia ya Yesu Kristo (Wagalatia 3:13, 14, 29)
-Yesu Kristo alipokuwa anatahiriwa, ilikuwa ni ishara ya kuwa damu yake ina nguvu ya kutuweka mbali na mapokeo ya dini yaliyo kongwa juu ya shingo za watu! Damu ya Yesu ina uwezo wa kutuingiza katika uhusiano na Mungu, kwa njia ya agano jipya! Kwa hiyo, damu ya Yesu inaweza kutumika kuondoa kile kinachofanya wakristo washindwe kushirikiana vyema, kwa sababu tu ya tofauti za mapokeo yao!

1 comment:

  1. Kristo Yesu asante kwa mafunuo ya haki yangu.amina mbarikiwe sana watumishi wa Mungu

    ReplyDelete

Injili ya Yesu Kristo Designed by INNJILI TANZANIA Copyright © 2013-2015

Injili Tanzania Blog. Theme images by Jason Morrow. Powered by Blogger.