VICHWA MBALIMBALI

KUFUNGA NA KUOMBA

Kufunga na kuomba nai sehemu muhimu sana katika maisha ya mkristo yoyote. Watu wengine huuliza kuwa je ni lazima kufunga? na kwanini nifunge?. Tuangalie kwa pamoja biblia inasemaje, kwanini tufunge.

1. Tunafunga kuonyesha utii kwa neno la Mungu (Yoeli 2:12)

Biblia kuanzia agano la kale hadi agano jipya inaonyesha umuhimu wa kufunga. Watumishi wote wa Mungu walikuwa wanafunga katika siku za maisha yao hivyo unavyofunga unaonyesha utii katika kulifuata neno la Mungu na kuliamini. Yesu Pia alisema kuwa siku zinakuja ambapo tutalazimika kufunga. (Mathayo 9:15)


2. Tunafunga ili kujinyenyekeza mbele za Mungu na kupata nguvu na neema yake

Tunahitaji neema ya Mungu siku zote ili tuweze kuishi, na ili kuipata inatubidi kujinyenyekeza chini ya mkono wake ulio hodari, Ebrania 4:16, Yakobo 4:10. Ezra aliwaamuru watu wafunge ili wapate kujinyenyekeza mbele za Mungu na kupata neema yake kwa ajili ya taifa lao, Ezra 8:21.

3. Tunafunga ili kuomba rehema

Yesu alichukua dhambi zetu zote msalabani, inawezekana kuna jambo unaona unashindwa kuacha na umejaribu sana. Hapo unatakiwa kufunga na kuomba rehema ili Mungu akuwezeshe kushinda. Pia unafunga kuomba rehema kwa ajili ya wengine mfano familia, jamaa na taifa pia. Daniel alifunga na kuomba rehema kwa ajili ya dhambi za taifa la Israeli na kubeba uovu wao mbele za Mungu. Danieli 9:3-5. Taifa la Ninawi walifunga na kuomba rehema kwa Mungu kutokana na uovu wao. Yona 3:5-10

4. Tunafunga ili katika udhaifu wetu Nguvu ya Mungu ionekane

Unapofunga unakuwa umeikana nafsi na kumchagua Mungu, uankuwa umedhamiria moyoni kutaka kuona nguvu ya Mungu ikionekana na sio nguvu yako. Zaburi 109:24-28, 2Korintho 12:9-10

5. Tunafunga kupata msaada wa Mungu katika kukamilisha kusudi lake

Viongozi wa kanisa la Antiokia walifunga na kuomba kabla ya kuwatuma Paulo na Barnabas. Walifanya hivi ili waweze fanya uchaguzi sahihi chini ya uongozi wa Mungu. Na Paulo na Barnabas walikuwa wakifanya hivyo katika miji waliyotembelea kila walipokuwa wanataka kuchagua viongozi. Kutokana na jambo hili makanisa yale yalizidi kusonga mbele maana walimshirikisha Mungu kwa kufunga katika maamuzi yao yote. Matendo 13:3-4, 14:23

6. Tunafunga wakati wa taabu

Mordekai na Esta walitangaza kufunga kwa wayahudi wote pale ilipofam=hamika kuwa kuna mpango wa kuwateketeza wayahudi wote, na kupitia kufunga na kuomba huku wayahudi walisalimika. Ester 4:15-16. Wakati wa taabu ni wakati wa kufunga na kumlilia Mungu na hakika Mungu ataonekana. Mfalme Yehoshafati pia alitangaza kufunga pale walipokuwa wamevamiwa na maadui wengi na wao hawakuwa na uwezo wa kupigana nao. 2Nyakati 20.

Tumeona kwa uchache jinsi kufunga kulivyo muhimu katika maisha yetu ya kila siku.

1 comment:

Injili ya Yesu Kristo Designed by INNJILI TANZANIA Copyright © 2013-2015

Injili Tanzania Blog. Theme images by Jason Morrow. Powered by Blogger.